Monday, 18 January 2016

SERIKALI YA BURUNDI NA UPINZANI KUKAA MEZA MOJA YA USULUHISHI.


Picha na maktaba.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litaishinikiza serikali ya Burundi kuzungumza na upinzani chini ya mpatanishi mpya, wakati wajumbe wa baraza hilo watakapoizuru nchi hiyo wiki hii, hayo ameyasema mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi. 
 
Mjumbe huyo, Jamal Benomar amesema mazungumzo yatapaswa kuongozwa bila kuegemea upande wowote na kuwekewa muda unaoeleweka, baada ya upatanishi wa Uganda kushindwa kupata muafaka wa kumaliza miezi kadhaa ya ghasia. 
 
Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa utawasili nchini Burundi Ijumaa wiki hii, ikiwa ziara ya pili ya baraza hilo nchini humo katika muda usiofika mwaka mmoja, katika juhudi za kuepusha kile kinachohofiwa kuwa uwezekano wa nchi hiyo kutumbukia katika vita vingine.
 
 Burundi iliingia katika mzozo wa kisiasa, baada ya rais wake Pierre Nkurunziza kugombea muhula wa tatu wa urais, ambao upinzani umesema ni kinyume cha katiba ya nchi hiyo.

0 comments:

Post a Comment

 

COPYRIGHT © Jicho Duniani DESIGN BY DISMAS TEN 0713216125