Watu wawili wamepigwa riasasi na kuuawa leo, katika makabiliano na polisi katika mji mkuu wa Burundi Bujumbura, wakati maandamano yakipamba moto kupinga hatua ya rais Pierre Nkurunziza kugombea muhula wa tatu.
Vurugu zimezuka katika maeneo kadhaa ya Bujumbura, siku moja baada ya chama tawala cha CNDD-FDD, ambacho kimetuhumiwa kwa kuwakandamiza wapinzani wake, kumtangaza rais Nkurunziza kuwa mgombea wake katika uchaguzi wa Juni 26 hapo jana.
Watu walioshuhudia wamesema mtu mmoja aliuawa katika wilaya ya Ngagara na mwingine katika wilaya ya Musaga, baada ya polisi kufyatua risasi za moto kuwatawanya watu waliokaidi marufuku ya serikali, na pia kuonya kuwa jeshi litaingilia. Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa watu wengine wengi wamejeruhiwa mjini humo, pamoja na maaskari kadhaa wa polisi.
Maafisa wamesema kituo maarufu cha redio - African Public Radio RPA, ambacho kimekuwa msitari wa mbele kuripoti ukandamizaji wa wapinzani, pia kimetishiwa kufungiwa kisipoacha kurusha matangazo ya moja kwa moja.
0 comments:
Post a Comment