Mkuu wa jeshi la Burundi jenerali Prime Niyongabo amesema leo kwamba jaribio la mapinduzi limeshindwa na majeshi tiifu kwa rais Pierre Nkurunziza yamepata udhibiti lakini mapigano makali katika mji mkuu Bujumbura yanaashiria kwamba mapambano ya kuwania udhibiti bado hayajamalizika.
Milio ya risasi na mabomu ilisikika kutoka eneo la makao makuu ya shirika la utangazaji la taifa. Radio ya taifa pamoja na televisheni vilizimika kwa muda , lakini hivi sasa matangazo hayo yako hewani.
Muda mfupi kabla ya matangazo kusita, rais Pierre Nkurunziza amewasifu wanajeshi tiifu kwake na ametoa msamaha kwa wanajeshi wanaompinga.
Hakuna taarifa rasmi juu ya mahali alipo Nkurunziza , lakini duru nchini Tanzania zinasema yuko mahali salama.
Pierre Nkurunziza alikuwa nchini Tanzania kwa mkutano wa viongozi wa eneo hilo uliopangwa kufanyika jana.
0 comments:
Post a Comment