Thursday, 26 May 2016

JINAMIZI LA KUZAMA BAHARINI BADO LINAWAANGAMIZA WATU MEDITERANIAN.



Mamlaka nchini Italia zinasema boti moja ya wahamiaji imezama kwenye Bahari ya Mediterenia hivi leo, siku mbili tu baada ya mkasa mwengine kama huo. Msemaji wa jeshi la walinzi wa pwani ya Italia anasema hadi sasa watu 88 wameokolewa, huku idadi kamili ya waliopoteza maisha ikiwa haijajulikana. Meli za uokozi za Umoja wa Ulaya zimethibitisha kuopoa maiti 20 hadi sasa. 
Hata hivyo, shirika la habari la Ansa limesema kiasi cha watu 30 wamefariki dunia kutokana na ajali ya leo. Katika boti iliyozama hapo jana, watu watano walithibitika kufa maji. Idadi ya boti za wahamiaji imepanda sana wiki hii, kutokana na kuanza kwa majira ya kiangazi na pepo za matilai. Jumla ya operesheni 20 za uokozi zinaendelea. 
Hadi juzi, Jumanne, idadi ya wahamiaji waliokwishawasili kwenye fukwe za Italia ilikuwa imeshuka kwa asilimia 9, lakini bado serikali inahaha kupata mahala pa kuwaweka wahamiaji zaidi ya 115,000 ambao tayari wamo nchini humo.

0 comments:

Post a Comment

 

COPYRIGHT © Jicho Duniani DESIGN BY DISMAS TEN 0713216125