Tuesday, 8 March 2016

BARA LA AFRIKA HUPOTEZA DOLLAR 150 ZA MAREKANI KILA MWAKA KUTOKANA NA RUSHWA.

 
 
WAZIRI MKUU wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema tatizo la rushwa barani Afrika limesababisha bara hilo lipoteze dola za Marekani bilioni 150 kila mwaka.


Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Machi 8, 2016) wakati akihutubia wajumbe wa mkutano wa tano wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) linaloendesha vikao vyake jijini Dar es Salaam. Mkutano huo ulioanza Machi 6, utamalizika Machi 18, mwaka huu.


Akizungumza kwa niaba ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu alisema rushwa imechangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya Jumuiya hiyo. "Rushwa yaweza kuwa kwa njia kuhonga fedha, kupata fedha kwa kula njama, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, ama kwa njia za vitisho," alisema.
"Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Afrika (AU), rushwa na urasimu vimeainishwa kuwa ni vikwazo vikubwa vinavyochangia kuchelewesha ufanyaji wa biashara kwenye mipaka ya nchi za Jumuiya yetu," alisema.
Amesema sekta binafsi inachukuliwa kama injini ya maendeleo na ukuaji wa uchumi na akatumia fursa hiyo kuipongeza jumuiya ya wafanyabiashara wa Afrika Mashariki kwa kuandaa kanuni za kiutendaji ambazo zimelenga kuhamasisha uadilifu kwenye ufanyaji biashara unaozingatia haki za binadamu, sheria za kazi, utunzaji mazingira na vita dhidi ya rushwa.
 
Akizungumzia kuhusu uondoaji wa vikwazo visivyohusisha kodi (non-tariff barriers) kama njia mojawapo ya kuimarisha biashara kwenye jumuiya hiyo, Waziri Mkuu alisema kwa upande wa Tanzania, vizuizi vya barabarani kwenye barabara kuu ya Kaskazini vimepunguzwa kutoka 50 hadi vitano.


Alivitaja vizuizi vitano vilivyobakia kuwa ni vile vilivyopo kwenye mizni ya Mikese (Morogoro), Nala (Dodoma), Njuki (Singida), Mwendakulima (Shinyanga) na Nyakahura (Kagera).


"Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya uondoaji wa vikwazo visivyohusisha kodi ilipitishwa Machi 2015 na sasa hivi inaendelea kusainiwa na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Pamoja na mambo mengie, nia ya sheria hii ni kuondoa vikwazo vinavyosababisha uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi na uuzaji wa bidhaa nje ya nchi, kurahisisha sheria za biashara ndani ya Jumuiya yetu," alisema.


Akizungumzia kuhusu miradi ya uwekezaji ya Jumuiya hiyo, Waziri Mkuu alisema miradi ya ujenzi wa barabara inahitaji kiasi cha dola za marekani bilioni 20; ukarabati na upanuzi wa njia za reli unahitaji dola za marekani bilioni 30; uendeshaji wa mashirika ya ndege na viwanja vya ndege unahitaji dola za marekani bilioni 15; uendelezaji bandari na usafiri wa majini unahitaji dola za marekani bilioni 10; utekelezaji wa miundombinu ya nishati inahitaji dola bilioni 5 ambavyo kwa pamoja vinahitaji dola marekani bilioni 80.


Alisema kuwepo kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi ndani ya jumuiya hiyo, kunaifanya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhesabika kuwa ni jumuiya yenye nguvu kubwa ya kiuchumi barani Afrika.

0 comments:

Post a Comment

 

COPYRIGHT © Jicho Duniani DESIGN BY DISMAS TEN 0713216125